Jana tarehe 08 Januari 2026, Ntemi Makwaia III wa XXIII wa Busiya alifanya ziara rasmi katika Kata ya Kolandoto akiwa ameambatana na ujumbe wake. Ziara hiyo ilipokelewa na Kiongozi wa Kata pamoja na Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa, ambapo walifanya kikao cha kwanza na Mkuu wa Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto, Ndg. P. S. Bujiku.
Katika ziara hiyo, Ntemi alitembelea jengo la kihistoria lililopo katika eneo la chuo, ambalo hapo awali lilikuwa wodi ya kwanza ya wazazi (maternity ward). Jengo hilo lina historia kubwa kwani ndilo lililowezesha kuzaliwa kwa wazazi wetu pamoja na watu wengi mashuhuri katika jamii. Kwa sasa, jengo hilo limebakia katika hali ya chakavu na lilikuwa karibu kuvunjwa, isingekuwa kwa kuthamini kumbukumbu na historia yake.
Jengo hilo lilijengwa na Ntemi Makwaia I, na kutokana na umuhimu wake wa kihistoria na kielimu, Ntemi Makwaia III ameahidi kutafuta wadau na watu wenye nia ya kuliboresha ili litumike kama Resource Centre ya Chuo cha Sayansi za Afya Kolandoto. Uongozi wa chuo na viongozi wa eneo hilo wamepokea na kuridhia wazo hilo kwa matumaini makubwa ya kuendeleza elimu na kuhifadhi historia ya eneo hilo.


